ZIARA YA MAKAMU WA PILI WA RAIS, SERA, URATIBU NA BARAZA LA WAWAKILISHI

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdallah amewapongeza watendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea kuifanya juu ya uratibu wa shughuli za kukabiliana na Maafa nchini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliyasema hayo leo Jumanne 24/11/2020 wakati alipofanya ziara katika ofisi za Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa huko Maruhubi Zanzibar.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdallah aliueleza Uongozi na watendaji wote  kwamba amefurahishwa sana na utendaji wa ofisi hiyo kwa kuwa yapo maendeleo kwa hatua fulani yaliofikiwa na kamisheni ya kukabiliana na Maafa.

Alisema kuwa ni wajibu wa kila mtumishi wa serikali kufanya kazi kwa bidii ili kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Dr. Hussein Ali Mwinyi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ili kuweza kufikia malengo tuliojiwekea.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Ndugu, Makame Khatib Makame alieleza yapo baadhi ya mafanikio mbalimbali ambayo yamefikiwa na kamisheni ya kukabiliana na Maafa kama vile Uboreshaji wa Mawasiliano kwa kutoa fursa kwa wananchi kupiga nambari ya simu bure wakati wa tukio lolote linaloashiria kutokea kwa maafa, sambamba na hilo kuongeza vituo vya mawasiliano Unguja na Pemba, kuendelea kutoa Elimu kwa Jamii, lakini pia Kusimamia Vizuri ujenzi wa Mradi wa Vijiji vya Makaazi ya waathirika wa mvua za masika za mwaka 2017 vilivopo Nungwi kwa Unguja pamoja na Tumbe kwa upande wa Pemba.

Aliipongeza, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutekeleza baadhi ya miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa misingi ambayo imesaidia kikamilifu kupunguza athari zinazopelekea maafa.

Aliendelea kueleza kuwa Sekretarieti ya Kamisheni ya kukabiliana na Maafa inaendelea kutekeleza kazi zake za kila siku za kukabiliana na Maafa Nchini mbali na kuepo kwa baadhi ya changamoto zinazoikabili ofisi hiyo.

Imetolewa na Kitengo cha Uhusiano.
KAMISHENI YA KUKABILIANA NA MAAFA ZANZIBAR