About Us


Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa ipo chini ya Mwenyekiti wake Makamu wa Pili wa Rais na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais anakuwa Makamu Mwenyekiti. Wajumbe wa Kamisheni Mawaziri wote wa SMZ, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama waliopo Zanzibar na Wakuu wa Mikoa yote ya Zanzibar. Katibu Mkuu wa Wizara inayosimamia maafa anakuwa ndie katibu wa Kamisheni.

 

Katika kutekeleza majukumu ya kila siku ya Kamisheni, imeanzishwa Sekreterieti ya Kamisheni inayoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji. Sekreterieti ya Kamisheni ina jumla ya Idara kuu tatu (3) ambazo ni Idara ya Mipango, Utawala na Rasilimali Watu, Idara ya Operesheni na Huduma za Kibinaadamu na Ofisi ya uratibu Pemba.

 

Aidha, kutakuwa na vitengo vikuu sita ambavyo vitasimamiwa moja kwa moja na Mkurugenzi Mtendaji. Vitengo hivyo ni Sheria, Uhusiano, Ukaguzi wa ndani, Uhasibu, Ununuzi na Ugavi pamoja na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Mbali na Muundo huo kutakuwa na Kamati za Kitaalamu ya Kitaifa na za Wilaya, Kamati za Kukabiliana na Maafa za Wilaya na Shehia.

 

1.3 Dira

Kupunguza athari za maafa kwa maisha ya watu na mali zao kwa kuchukua hatua madhubuti za kujikinga, kujitayarisha, kukabiliana na kurudisha hali baada ya maafa kutokea.

 

1.4 Dhamira

Kuwa na njia bora zitazopunguza matukio yanayoweza kusababisha upotevu wa maisha ya watu na mali zao.

 

1.5 Lengo

Kamisheni hii imeanzishwa kwa lengo la kuimarisha mfumo wa uratibu wa shughuli zote za kukabiliana na maafa kwa kuiwezesha jamii kuhimili majanga na maafa hapa Zanzibar kupitia misingi mikuu iliyokubalika kikanda na kimataifa katika kupunguza, kujiandaa, kukabili na kurejesha hali baada ya maafa kutokea.

 

1.6 Majukumu makuu ya Kamisheni

Kamisheni itakuwa na majukumu yafuatayo:-

 

 1. Kuanzisha sera za kukabiliana na maafa, kanuni, mipango, mikakati na miongozo ili iweze kukabiliana na maafa kwa wakati na ufanisi;
 2. Kuwezesha upatikanaji wa fedha na rasilimali nyengine wakati wa dharura na/au maafa;
 3. Kusimamia utekelezaji wa mipango ya kukabiliana na maafa wakati wa maafa ya asili au dharura na kutoa amri au maelekezo yanayofaa kwa utekelezaji wa mpango huo;
 4. Kuratibu huduma za utoaji wa misaada ya kibinadamu pamoja na hatua za kujiandaa katika kukabiliana na maafa;
 5. Kuwa na jukumu la kusimamia na kuratibu kazi za kukabiliana na maafa nchini;
 6. Kupendekeza utaratibu wa upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kukabiliana na maafa;
 7. Kuimarisha uwezo wa Serikali katika kusimamia hali za dharura na/au maafa;
 8. Kuangalia uwezekano wa upatikanaji wa rasilimali ndani na nje ya Zanzibar ili kukabiliana na maafa kwa ufanisi;
 9. Kuhakikisha uwajibikaji wa taasisi muhimu katika utekelezaji wa Sheria ya Kukabiliana na Maafa Nam. 1 ya mwaka 2015;
 10. Kuhakikisha utekelezaji wa sera za Serikali, sheria, mipango na kazi za kukabiliana na maafa zinaendana na makubaliano pamoja na mikataba ya Kikanda na Kimataifa;
 11. Kuhakikisha kuwa taasisi za Serikali, Wilaya na Shehia zinakuwa na uwezo wa  kukabiliana na maafa kupitia utoaji wa mafunzo na vifaa; na
 12. Kufanya kazi yoyote ambayo Kamisheni itaona inafaa katika kutekeleza shughuli za kukabiliana na maafa.