SERIKALI YA MAPINDUZI ZANZIBAR INAENDELEA KUCHUKUA HATUA ZA MSINGI KATIKA KUKABILIANA NA MAJANGA ILI KUWALINDA WANANCHI NA ATHARI ZINAZOWEZA KUJITOKEZA.

Akifungua Mkutano wa Uwasilishaji wa Ripoti ya Tathmini ya Mahitaji juu ya Uiamarishaji wa Mifumo ya Kielektroniki katika Kukabiliana na Maafa kwa niaba ya Makamu wa Pili wa Rais huko katika Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa ndege Zanzibar, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Mhe. Hamza Hassan Juma amesema juhudi hizo ni pamoja na kutoa tahadhari za mapema kwa wananchi, kuboresha huduma za mawasiliano ikiwemo kutumia tehama ili waweze kuchukua tahadhari na kuepukana na athari zinazoweza kujitokeza kabla na baada ya majanga kutokea.

"Tathmini hii inaonesha hali halisi tulivyo na mahitaji yetu katika kuimarisha mifumo ya kielektroniki katika kukabiliana na maafa kabla maafa hayajatokea, wakati na baada ya maafa kutokea kwa misingi ya kujikinga au kupunguza athari, kujiandaa, kukabiliana nayo na kurejesha hali kwa wananchi wetu baada ya maafa."

Nae, Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Ndg. Makame Khatibu Makame ameeleza kuwa, kuwepo kwa mfumo huo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupata taarifa za mapema na kutoa wito kwa wananchi kufuatilia kwa karibu taarifa zinazotolewa na mamlaka husika katika kukabiliana na maafa.

"Uwepo wa masuala ya mifumo katika kukabiliana na maafa ni suala la msingi ambapo litawezesha jamiii kupata taarifa kwa haraka katika maeneo yote muhimu ya kujikinga, kupunguza athari, kujiandaa na kukabiliana na maafa pamoja na kurejesha hali baada maafa kutokea".

Aidha, Washiriki wa Mkutano huo wamesema kuna umuhimu mkubwa sana wa kuunganisha mifumo ya mawasiliano katika kutoa taarifa za dharura ili kuwapa wepesi wanchi.

Mkutano huo umewashirikisha wadau mbalimbali kutoka Serikalini, Jumuiya za Maendeleo, Sekta Binafsi na Asasi za kiraia.

 

KAMISHENI YA KUKABILIANA NA MAAFA.

20 OKTOBA 2022