SERIKALI ITAENDELEA KUVIIMARISHA VITUO VYAKE VYA UOKOZI ILI KUKABILIANA NA MAAFA” MHE. HEMED SULEIMAN ABDULLAH

“SERIKALI ITAENDELEA KUVIIMARISHA VITUO VYAKE VYA UOKOZI ILI KUKABILIANA NA MAAFA” MHE. HEMED SULEIMAN ABDULLAH

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kuchukua tahadhari za kuwakinga wananchi  wake na majanga mbalimbali kwa kutoa elimu ya kuepuka mazingira  hatarishi yanayoweza kusababisha maafa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla alieleza hayo katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Maafa duniani hafla iliyo fanyika  katika ukumbi wa Shekh Idriss Abdulwakili kikwajuni jijini Zanzibar.

Mhe. Hemed alisema katika kuhakikisha azma hiyo inafanikiwa Serekali itaviimarisha vituo vyake vya uokozi vinavyo simamiwa na kikosi cha zima moto na uokozi pamoja na vituo vya uokozi vinavyo simamiwa na kikosi maalumu cha kuzuia magendo (KMKM) kwa kuvipatia nyenzo za kukabiliana na maafa barani na baharini.

Alisema Zanzibar ikiwa nchi ya visiwa imekuwa ikikumbwa na majanga tofauti yanayo pelekea maafa ambapo alisema kwa mujibu wa tathmini iliyofanywa na kamisheni ya kukabiliana na maafa Zanzibar jumla ya nyumba Elfu kumi na arubaini na tatu (10,043) ziliathiriwa kutokana na mafuriko ya mwaka jana na watu wanane walifariki, pia matukio mia moja thalathini na mbili (132) ya moto yaliripotiwa kuanzia mwezi wa Januari hadi Septemba mwaka huu 2021.

Aidha,Mhe Hemed  alieleza maafa  yatokanayo na ajali imeendelea kuwa changamoto ambapo jumla ya ajali Mia moja na hamsini na sita (56) za barabarani ziliripotiwa kwa kipindi cha Januari hadi Septemba mwaka huu ambapo ajali Mia Moja na tisa (109) zimesababisha vifo vya watu Mia moja na ishirini na nane (128).

 

Pamoja na mambo mengine Mhe. Hemed amelitaja janga la maradhi ya covid _19 kusababisha maafa na kua tishio duniani ambapo kwa Zanzibar jumla ya wagonjwa Elfu nne mia tatu na arubaini na tano  (4,345) wamethibitishwa kuwa na UVIKO-19 kwa kipindi cha mwezi  April hadi Septemba 2021 ambapo vifo sitini na saba (67)vimethibitishwa.

Katika kadhia hiyo Mhe. Hemed  aliendelea kutoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari kwa kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya ikiwemo kupata chanjo inayotolewa bure na serekali.

Katika hatua nyengine Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema serekali imelenga kutumia mifumo ya Teknolojia ya mawasiliano ikiwemo kuanzisha kituo cha mawasiliano ya dharura (Emergency Call Center) kupitia namba ya 190 ambayo inawapa fursa wananchi wake kupiga simu bure “Nawaomba wananchi muitumie vizuri namba hii ya dharura katika kipindi hichi cha majaribio” Alisema Mhe.Hemd.

Makamu wa Pili wa Rais aliagiza kamisheni ya kukabiliana na maafa na Wizara ya Ujenzi ,Mawasiliano na Uchukuzi kuharakisha zoezi la kuunganisha mifumo katika sekta zinazohusika  ili kurahisisha  upatikanaji wa mawasiliano na kutumia rasilimali zilizopo kwa ajili ya kukabiliana na majanga.

Akizungumzia suala la uchumi wa buluu Mhe. Hemed alieleza serekali ya awamu ya nane imeweka mkazo katika sekta hiyo, hivyo serekali imeufanyia mapito mpango wa Taifa wa kujiandaa na kukabiliana na maafa(Emergency Preparedness and Response Plan)ili iendane na hali halisi iliopo sambamba na kuandaa mfumo wa kutoa na kupoke taarifa za mapema ikwa ni pamoja  na kutuma ujumbe  mfupi ya (sms) ili kuifikia jamii kubwa ya wazanzibar wakiwemo wavuvi na wakulima.

Kwa upande wake kaimu Waziri, Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera uratibu na Baraza la wawakilishi Mhe. Haroun Ali Suleiman alitaka jamii kuchukua tahadhari kwa kuufanyia kazi ujumbe wa mwaka huu ili kuendelea kujikinga na maafa.

Mhe.Haroun alieleza kuwa mazingira yanayo wazunguka wananchi  sio ya kuridhisha hali inayosababisha  watu kuishi katika hali hatarishi  ambapo alitumia fursa hiyo kuwaomba wasimamizi wa Wilaya,Mikoa na majimbo kuufikisha na kuufanyia kazi ujumbe huo juu ya kukabiliana na majanga mbalimbali katika maeneo yao.

Nae katibu Mkuu Wizara ya Nchi Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais Ndugu Thabit Idarusi Faina alieleza Wizara kupitia Kamisheni ya kukabiliana na Maafa katika kuanzisha siku hii imechukua jitihada mbalimbali ikiwemo kuandaa makala mbalimbali, kutoa elimu ya kukabiliana na maafa  kwa wanafunzi kupitia skuli tofauti.

Pia katibu Faina alisema Wizara inaendelea kushirikiana na Taasisi mbalimbali za ndani na Nje ya nchi kwa kushiriki mikutano na makongamano  kwa ajili ya kusaidia kuimarisha mfumo wa kukabiliana na maafa.

Ujumbe wa mwaka huu katika kuadhimisha siku ya maafa dunuani “KWA PAMOJA TUNAWEZA KUIKOA DUNIA DHIDI YA MAAFA”

 

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)

Oktoba 13, 2021.