SMZ KUJA NA MIPANGO NA MIKAKATI MADHUBUTI KATIKA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIA NCHI

Mkurugenzi Mtendaji Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa ameongoza kikao cha warsha pamoja na wadau wa kukabiliana na maafa lengo hasa likiwa ni kujadili juu ya suala la kujenga uhimili katika masuala ya Mabadiliko ya Tabia nchi.  


Katika warsha hiyo wadau mbali mbali walipata fursa ya kushiriki wakiwemo Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Kanda ya Zanzibar, Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira, Wizara ya Kilimo, Mamlaka ya maji Zanzibar (ZAWA) na Idara ya Mipango Miji ambapo jumla ya mada tatu ziliwasilishwa na kuchangiwa kuhusiana na masuala ya Utabiri wa Hali ya hewa, Mabadiliko ya Tabia nchi pamoja na masuala ya Kukabiliana na Maafa.


Hata hivyo, kutokana na umuhimu mkubwa uliopo kwa nchi yetu ya kuwa na mipango na mikakati madhubuti ya kukabiliana na suala la Mabadiliko ya Tabia nchi. kikao hicho kimetoka na azimio la kuundwa kamati ndogo yenye wajumbe kutoka taasisi muhimu kwenye masuala ya mabadiliko ya tabia nchi lengo likiwa ni kuandaa dhana ya msingi ya utekelezaji wa mpango huo wa kujenga uhimili wa masuala ya mabadiliko ya Tabia nchi.

 

Picha na Abubakar Mzee Ibrahim-Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar 

Agosti, 28, 2021.