KAMISHENI YA KUKABILIANA NA MAAFA INA LENGO LA KUWEKA UTARATIBU MZURI WA KUKABILIANA NA MAAFA YANAYOWEZA KUTOKEA NCHINI.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa iliopo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Ndugu Makame Khatib Makame ameyasema hayo wakati akifungua kikao na wadau wa maafa cha kupitia Rasimu ya Kanuni za Kukabiliana na Maafa Zanzibar za mwaka 2021 na Kanuni za Mfuko wa Kukabiliana na Maafa Zanzibar za mwaka 2021 kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi za Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Maruhubi Mjini Zanzibar.

Ameeleza kuwa kumekuwepo na majanga mbalimbali yanayopelekea maafa ambayo huwakumba wananchi kila siku kama vile ajali za moto, ajali za barabarani, mafuriko, NK, hivyo kanuni hizi zimelenga katika maeneo mbalimbali zitaweza kusaidia kuleta ufanisi katika shughuli za kukabiliana na maafa nchini.

Nae, Afisa Sheria kutoka Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Ndugu Thureya Ghalib Mussa akiwasilisha Rasimu hizo kwa wajumbe wa kikao hicho ambao ni wadau wa maafa kutoka katika Taasisi mbalimbali za Serikali na Taasisi binafsi ameeleza kuwa kila mdau ana nafasi ya kutoa michango ya kuziboresha rasimu ya kanuni hizo.

Aidha, Kanuni hizo zimeundwa kwa kifungu cha 47 cha Sheria ya Kupunguza na Kukabiliana na Maafa Nam 1 ya 2015 ambapo zitaanza kutumika rasmi mara baada ya kusainiwa na Waziri na kutangazwa katika Gazeti Rasmi la Serikali.