NUNGWI KASKAZINI UNGUJA 01/03/2021: MAKABIDHIANO YA VIJIJI VYA WANANCHI WALIOATHIRIWA NA MVUA ZA MASIKA ZA MWAKA 2017.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekabidhiwa nyumba 60 kwa ajili ya wananchi walioathiriwa na mvua za masika za mwaka 2017, ambazo zimejengwa Nungwi kwa Unguja na Tumbe kwa upande wa Pemba kwa msaada wa Jumuiya ya Falme za Kiarabu ya Mwezi Mwekundu. (Emirates Red Crescent).

Akitia saini hati ya makabidhiano hayo kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Ndugu Thabit Idarous Faina na Sheikh Said Alqumari kwa upande wa Jumuiya ya Falme za Kiarabu ya Mwezi Mwekundu. (Emirates Red Crescent).

Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Dr. Khalid Salum Mohammed alisema nyumba hizo zitaweza kuwapa makaazi bora na salama wananchi wa Zanzibar waliopatwa na janga hilo, huku akisifu Juhudi za wakandarasi kukamilisha mradi huo kwa wakati uliopangwa.

“Pamoja na yote haya kazi hiii tumeifanya kwa mashirikiano makubwa, tumeifanya kwa mashirikiano makubwa baina ya wenzetu wa UAE, lakini hasaa Red Crescent wamefanya kazi kubwa, lakini pia maengineer wamefanya kazi kubwa, mkandarasi amefanya kazi kubwa, mshauri muelekezi amefanya kazi kubwa sana”

Nae, Balozi wa Falme za Kiarabu nchini Tanzania Mhe. Khalifa Abdulrahman ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwakubalia kutimiza azma yao ya kujenga nyumba hizo na kuahidi kuendelea kuunga mkono shughuli mbalimbali za maendeleo nchini.

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud alisema kazi iliofanywa na umoja huo ni ya kupigiwa mfano na amewakaribisha kuwekeza na kutoa misaada zaidi ndani ya mkoa huo.

 

KITENGO CHA UHUSIANO

KAMISHENI YA KUKABILIANA NA MAAFA ZANZIBAR.