Salam za Mkurugenzi Mtendaji, Makame Khatib Makame

SALAMU ZA MKURUGENZI MTENDAJI

WA KAMISHENI YA KUKABILIANA NA MAAFA

Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa ni Taasisi iliyo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais ambayo inajukumu la msingi la kuratibu masuala yote ya Kukabiliana na Maafa hapa Zanzibar pamoja na kuiwezesha jamii kujenga uhimili wa matukio mbalimbali ya kimaafa yanayoweza kutokea.

Nachukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu kwa kutuwezesha kuendelea kujenga uwezo wa jamii na wahusika mbalimbali katika kujikinga na kukabiliana na maafa kupitia tovuti hii. Aidha, napenda kuwashukuru wafanyakazi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa na wahusika kwa kufanikisha kukamilika kwa tovuti hii.

Kutokana na ongezeko la matukio ya majanga ya asili na yale yanayosababishwa na binadamu ambayo hupelekea maafa duniani kote, mahitaji ya kujenga uwelewa kwa jamii na wahusika wengine yanaendelea kukua hali inayopelekea umuhimu wa kuiwezesha kitaaluma na kimiundombinu. Katika kulifanikisha hilo, Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa imeanzisha tovuti hii kwa lengo la kutoa elimu ya kukabiliana na maafa kwa jamii na wahusika wengine.

Ni imani yangu kwamba jamii na wahusika mbalimbali wa maafa wataitumia tovuti hii katika kuimarisha misingi mikuu ya kukabiliana na maafa ambayo ni kujikinga, kupunguza athari, kujiandaa, kukabiliana na kurejesha hali baada ya maafa kutokea. Katika tovuti hii shughuli mbalimbali za Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa zimeainishwa pamoja na kuonesha matukio ya kimaafa na miongozo mbalimbali inayotumika katika kukabiliana na maafa hapa Zanzibar.

Mbali na uanzishwaji wa tovuti hii Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa imekuwa ikitoa elimu ya kukabiliana na maafa kupitia njia mbalimbali ikiwemo kuandaa vipindi vya redio na Tv, Makala za kuona (documentary), michezo ya kuigiza na matangazo mafupi.

Mwisho natoa wito kwa wananchi na wahusika mbalimbali kuitumia tovuti hii zikiwemo taasisi za Serikali na zisizo za Kiserikali kuendelea kuiuunga mkono tovuti hii na kuweza kuiimarisha ili kupunguza athari mbalimbali za kimaafa.